Ads 468x60px


KWANINI RANGI HUBANDUKA KWENYE UKUTA?


                                Ukuta uliobanduka rangi


    Mara nyingi tumekuwa tukiona rangi inachubuka au kubanduka kwenye kuta za majengo yetu, tatizo hili hukumba majengo mengi hata yakiwemo yale tunayoishi wenyewe. Watu wengi tumekuwa tukitatua tatizo hili kwa kupaka rangi nyingne juu ya ukuta uliobanduka rangi, na kumbe! Rangi hubanduka tena baada ya muda mfupi. Zifuatazo ni baadhi ya sababu zinazosababisha rangi kubanduka/kuchubuka kwenye.


SABABU ZA KUBANDUKA/KUCHUBUKA KWA RANGI.
·      
         Maandalizi mabovu ya eneo la kupaka rangi – kabla ya kupaka rangi kwenye ukuta inabidi eneo husika la kupakwa rangi liandaliwe vizuri. Mara nyingi tumekuwa tukikurupuka kupaka rangi kwenye eneo ambalo halijaandaliwa vizuri. Sehemu yeyote inayotarajiwa kupakwa rangi ni lazima iwe kavu, safi na isiwe na hali yeyote ya mafutamafuta.
Hii ni muhimu kwa eneo lolote, iwe ni ukuta uliopakwa plasta au mbao au chuma. Kama unatumia mbao hakikisha hali ya unyevu haipungui 18%, pia kuwe na sura nyororo iliyopigwa msasa. Kama ni chuma, hakikisha hakuna kutu na uso wa chuma usugliwe kwa kutumia brashi za waya.
Kwenye ukuta wa matofali ambao umemaliziwa kwa plasta, hakikisha plasta ipo katika hali nzuri- isiwe na vishimo, iwe kavu na safi, yaani isiwe na vumbi au hali ya umafuta, pia iwe imara.

·         Kutumia rangi ambazo ziko chini ya kiwango- hii mara nyingi huwa inatokea pale tunapotaka kubana bajeti kwa pesa iliyopo, tumekuwa tukichanganya maji mengi na rangi ili tuwe na rangi nyingi ya kupaka kwenye ukuta. Muda mwingine tumekuwa tukienda dukani na kuulizia rangi za bei rahisi kabisa.

·         Utendajikazi mbovu wakati wa upakaji rangi- hii mara nyingi huwa ni kosa la mafundi wetu tunaowatumia. Fundi akiwa sio mzoefu na kazi au asipokuwa makini mara nyingi huwa anafanya kazi iliyo chini ya kiwango.


·         Uandaaji mbaya wa rangi- mara nyingi tunaponunua rangi madukani, huwa tunapewa maelekezo jinsi ya kutumia, mara nyingi huwa hatuufuati huo ushauri, na hii mara nyingi husababishwa na mafundi ambao huwa wanajihisi wao ni wazoefu. Ni kweli kuwa rangi ni lazima ichanganywe na solvent ili kubadilisha hali yake ya uji-uji, lakini ni vizuri tukafuata maelekezo.

·         Kupaka rangi chini ya koti 3- ili rangi iweze kuwa imara na kushika kwenye ukuta, ni vyema zikapakwa koti 3(mara 3). Koti ya kwanza hupakwa kwenye eneo ambalo halijapakwa rangi kabisa mfano plasta, ili kuleta hali ya umurua kwenye ukuta. Koti ya pili hupakwa ili kupokea koti ya tatu ambayo ni ya finishing. Koti ya tatu ni kwa ajili ya mwonekano mzima wa ukuta na kuzuia ukuta na hali ya kulika.


·         Kutokujua sehemu za kutumia rangi za maji na mafuta- hili limekuwa likichanganya watu wengi,  na wengi wamekuwa wakijiuliza ni mahali gani sahihi kwa rangi ya aina gani. Maeneo yenye majimaji, mfano bafuni au jikoni, ni vizuri kutumia rangi za mafuta. Pia kuta zako kama ni rahisi kuchafuka, ni vizuri kutumia rangi za maji kwani ni rahisi zaidi kuzisafisha.

·         Kifaa kinachotumika kupakia rangi- kuna vifaa vikuu vitatu vya kupaka rangi kwenye jengo, navyo ni brashi, roller na spray. Vifaa hivi vitatu vinafanya kazi moja, ila kunaweza kuwa na tofauti katika mwisho wa kazi. Utendajikazi wa brush sio mzuri sana ukilinganishwa na wa roller au spray, pia roller na spray zinaokoa muda kuliko utumiaji wa brush.


·         Unyevu unaopanda kwenye ukuta kutoka ardhini- hii inaweza kuwa ni sababu kubwa zaidi inayosababisha rangi kuchubuka. Mara nyingi hii husababishwa na makosa yanayojitokeza  wakati wa ujenzi wa msingi na ukuta wa jengo. Wakati wa ujenzi wa msingi ni lazima kuwekwe kitu kinachuzuia unyevu kupanda kwenye ukuta, kwa kitaalamu inaitwa dump proof membrane. Hii husaidia unyevu kutopanda na kuharibu rangi kwenye ukuta.

Kama ukuta wako umechubuka au kubanduka rangi ni vyema kutoa kabiisa hata rangi iliyopo na kupaka rangi kwa upya. Hii husaidia kuwa na matokeo mazuri zaidi.

0 comments: